ads

WAKATI Wazanzibari leo wakiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein (pichani), amebainisha kuwa mapinduzi hayo ndio alama, sifa, ukombozi na uhuru wa raia hao wa visiwa vya Zanzibar.


Dk Shein amesema hana ugomvi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi na kubainisha kuwa wanatofautiana kisiasa, ni jambo la kawaida na mazungumzo ya muafaka yalishafanyika.

Pamoja na hayo, Rais huyo amebainisha kuwa anaamini amechaguliwa kihalali na Wanzanzibari, ambapo kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar mwaka 2015, hakukuwa na shinikizo lolote kutoka serikalini bali ni maamuzi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya kubaini mchezo mchafu kwenye uchaguzi huo.

Halikadhalika, Dk Shein amesema harakati za kuandaliwa kwa Katiba mpya ya Tanzania, zimefuata taratibu zote kwa mujibu wa Sheria na Katiba katika kipindi chake cha uongozi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na sasa kilichobaki ni kuendelea na mchakato wa kura za maoni na kutungwa kwa Katiba hiyo.

Dk Shein aliyasema hayo mjini Zanzibar jana wakati akihojiwa na televisheni ya Azam katika kipindi cha Funguka kuhusu maandalizi ya mapinduzi, utendaji wake kama Rais wa saba Zanzibar, uchaguzi wa Zanzibar na maendeleo ya mchakato wa Katiba.

Sherehe za Mapinduzi

Kuhusu sherehe za Mapinduzi, Rais huyo alisema Wazanzibari wanapaswa kujivunia kupatikana kwa mapinduzi hayo kwa kuwa ndio mkombozi na uhuru wao, hasa baada ya kupata mateso na manyanyaso ya kutawaliwa kutoka kwa watawala mbalimbali wakiwemo waarabu kutoka Oman.

Alisema Wazanzibari walitawaliwa tangu mwaka 1553 na Wareno kwa muda wa takribani karne mbili na baadaye Waarabu kutoka Oman kwa takribani miaka 40 hadi pale waasisi akiwemo Abeid Amani Karume, chini ya chama cha Afro Shiraz walipofanikisha mapinduzi na kuikomboa nchi hiyo.

Alisema enzi za ukoloni, Wazanzibari waliteseka ambapo pamoja na kuteswa pia walinyimwa haki ya kupata elimu, kumiliki ardhi ya nchi yao na kukosa fursa ya kupatiwa huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya.

“Hii ni miaka 53 ya uhuru na ukombozi wa Wazanzibari, kwetu sisi mapinduzi haya ni alama yetu, ndio sifa yetu, ndio uhuru na ukombozi wetu. Mapinduzi ndio ishara na njia iliyotukomboa na kutuweka huru na sasa tunajitawala wenyewe,” alisisitiza.

Uchaguzi Zanzibar

Kwa upande wa mgogoro ulioibuka wakati wa uchaguzi, Dk Shein alibainisha kuwa anaamini alichaguliwa kihalali na wazanzibar katika uchaguzi wa pili, uliofanyika baada ya wa kwanza kufutwa na ZEC na kusisitiza kuwa hakukuwa na mkono wowote wa serikali katika kushinikiza uchaguzi huo ufutwe.

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ZEC) ni tume huru zinazofanya kazi zake bila kuingiliwa na chombo chochote ikiwemo Serikali, ingawa wenyeviti wake wanateuliwa na Rais kwa mujibu wa Katiba.
“Naomba niweke wazi maamuzi ya tume yanafanywa na tume yenyewe, serikali haihusiki na maamuzi yoyote ya uchaguzi, ila serikali inahusika na gharama za uchaguzi,” alifafanua.

Aidha, Rais huyo alifafanua kwanini uchaguzi wa Zanzibar ulipoahirishwa haukugusa uchaguzi wa Bara na kubainisha kuwa pamoja na kuwepo tume zote mbili, ZEC na NEC, tume zote huwajibika kwa mujibu wa sheria na Katiba tofauti.

Alisema ZEC imekuwa ikifanya kazi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na Katiba ya Zanzibar na hata uchaguzi wake unahusu rais, wabunge, wawakilishi na mashehia, wakati NEC imekuwa ikisimamia nchi nzima ikiwemo Zanzibar na kwa Bara husimamia uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

“Uchaguzi uliofutwa ulikuwa chini ya ZEC kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Zanzibar na tume hii ilielezea sababu mbalimbali zikiwemo tisa za kufutwa kwa uchaguzi huo na uchaguzi uliofanyika upya uliofuata taratibu zote wakiwemo waangalizi kutoka sehemu mbalimbali,” alisema Dk Shein.

Mazungumzo na Maalim Seif

Akizungumzia mazungumzo yake na mpinzani wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema mazungumzo ya muafaka yalifanyika na yalienda vizuri, yakihusisha viongozi waandamizi akiwemo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar mstaafu Amani Abeid Karume.
Alisema katika mazungumzo hayo, kuliibuka kutofautiana kati yao, ambapo Maalim Seif aling’ang’ania kuwa hayuko tayari uchaguzi ufutwe na urudiwe wakati yeye Dk Shein aliiamini ZEC na kubainisha wazi kuwa endapo uchaguzi utarudiwa atashiriki.

“Kikao kilienda vizuri hakukuwa na uonevu wala upendeleo kwa upande wowote, ila hatukukubaliana. Kilichotokea katika uchaguzi ni muendelezo wa historia ya Zanzibar kila unapofanyika uchaguzi lazima kuwe na malumbano na vituko, upande mmoja huwa unakataa matokeo,” alisema.

Alisema sababu ya kufutwa kwa uchaguzi wa kwanza wa Zanzibar ni kutokana na kubainika kuwepo kwa dhuluma nyingi na hadaa katika uchaguzi huo.

Kuhusu kitendo cha Maalim Seif kuzunguka ndani na nje ya nchi, kuishtaki SMZ kwa kitendo cha kufuta na kurudia uchaguzi kwa madai ya kutokuwa na ridhaa ya Wazanzibari, Dk Shein alibainisha wazi kuwa kitendo hicho hakimshtui, kwa kuwa uchaguzi huo ulifanyika kihalali chini ya mamlaka ya ZEC.

Kero za muungano

Akifafanua kuhusu hoja za kero za muungano, rais huyo aliwataka watanzania wakiwemo wazanzibari, wajivunie kwa dhati muungano huo kwa kuwa ni nchi chache duniani zilizofanikiwa kutengeneza muungano na kudumu nao.

Alisema muungano uliopo, hauna tatizo lolote wala kero, kama inavyobainishwa na watu wachache wasioutakia mema muungano huo kwa sababu zao na kusisitiza kuwa wale wote wanaopinga muungano ni wazi kuwa hajui vyema historia yao na ya nchi zao.

“Waasisi wetu waliamua kuutunganisha baada ya kuona namna tulivyokuwa tunaishi, muungano huu ni wa kindugu zaidi. Na hata hizo kero zinazodaiwa kuwepo nyingi zimeanzishwa na watu wachache wenye malengo yao binafsi na si kuutakia mema muungano huu,” alisema.

Alitolea mfano kero ya mafuta inayozungumziwa na kuonyesha kushangaa kwa nini hoja hiyo inabuliwa kwa kuwa katika mkataba wa muungano suala la uchumi ni la nchi binafsi wala halipo kwenye muungano.

“Kwa sasa suala tunalolishughulikia mkataba wa kifedha tu na si kero kama inavyodhaniwa.” Katiba Kwa upande wa mchakato wa Katiba, unaotarajiwa kuendelea katika Serikali ya Awamu ya Tano, Dk Shein alibainisha kuwa mchakato huo wakati wa kipindi cha Kikwete ulikwenda vizuri kwa kupitia hatua kadhaa ikiwemo kutungwa kwa sheria ya Katiba, kuundwa kwa Tume ya Wajumbe wa Katiba, Bunge la Katiba na hatimaye kupatikana kwa rasimu. 

“Tulishirikiana vyema pande zote mbili za muungano, tumepitia hatua kwa hatua, na hata sasa katika serikali hii ya awamu ya tano, nina imani nitaendelea kushirikiana na Rais John Magufuli kuendeleza pale tulipoachia na kwenda kwenye hatua ya kura za maoni. Hapa ndio tutajua tuanze upya mchakato au tuendelee,” alisema.

Mafanikio ya Dk Shein

Akizungumzia mafanikio yake ya kuiongoza Zanzibar akiwa Rais wa saba ya visiwa hivyo, alisema amepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta kadhaa za kiuchumi, kielimu na kiafya.

Alisema anakwenda vizuri sambamba na kasi ya Dk Magufuli na falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu’, ambapo na yeye amekuwa akiwachukulia hatua watumishi na viongozi wasiowajibika na wanaotumia vibaya ofisi zao, ikiwemo kuwatumbua.

“Unajua vyombo vya habari vimejikita zaidi bara lakini kama vingekuwepo na kufuatilia utendaji wetu visingekuwa vinauliza kama kuna utumbuaji huku. Njooni muone wenyewe. Mimi kweli wananiita mpole, hiyo ni nature (asili) yangu lakini sivumilii mtu yeyote anayekwenda kinyume,” alisisitiza.

Leo Zanzibar inaadhimisha miaka hiyo 53 ya mapinduzi na sherehe zitafanyika katika uwanja wa Aman mjini Unguja na kuhudhuriwa na Dk Shein atakayepokea gwaride na heshima la vikosi vya ulinzi, vikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuvishirikisha vikosi vya idara maalumu vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo JKU,KMKM na Valantia.

Aidha Dk Shein atapokea maandamano ya wananchi wa mikoa 5 ya Unguja na Pemba ambayo watapita mbele ya mgeni rasmi kwa ajili ya kutoa salamu ya heshima huku wakiwemo wafanyakazi wa Wizara na taasisi mbali mbali za Serikali na sekta binafsi.

DOWNLOAD APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD BONYEZA HAPA  

ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: